Taasisi iitwayo ndoa ina magugu ambayo yasipoondolewa hudhoofika au kupata matatizo makubwa. Magugu yaliyoko kwenye ndoa yasiposhughulikiwa mapema na kwa dhati, ndoa hiyo huweza kuvunjika au kufa kabisa.
Je, ndoa yako inasumbuliwa na magugu? Bila shaka jibu ni ndiyo kwa sababu hakuna ndoa isiyokuwa na tatizo la aina fulani. Walivyosema wahenga, udongo uwahi ungali maji. Na wewe mwanandoa unaambiwa, magugu ya ndoa yawahi yangali machanga. Kwa hiyo, mawaidha yafuatayo ni dawa au viwatilifu ambavyo vitatokomeza magugu kwenye ndoa yako:
(i) Sahau wapenzi wa zamani. Wanandoa wengi siku hizi hulinganisha wenzi wao wa ndoa na wapenzi wao wa zamani. Wengine huwa na mahusiano ya siri na wapenzi hao wa zamani. Hili ni gugu baya sana katika ndoa.
Mwanandoa kuendelea kuhusiana na wapenzi wa zamani husababishwa na nini? Kwa kujibu swali hili tunaweza kusema kwamba mtu anayekula kwenye migahawa mingi anapoambiwa ale kwenye mgahawa mmoja tu huanza kulinganisha migahawa ya zamani na mgahawa wake mpya. Pia mtu aliyezoea kula kwa mama ntilie wengi anapoambiwa apikiwe na mtu mmoja tu huwa vigumu sana kwake kuacha kulinganisha mpishi wake mpya na wale mama ntilie aliozoea kula kwao.
(ii) Ridhika na mwenzi wako wa ndoa. Kutokuridhika na mwenzi wako wa ndoa ni gugu. Kwa nini wanandoa wengi hawaridhiki na wenzi wao wa ndoa? Wataalamu wa masuala ya ndoa hueleza kwamba hakuna mtu mkamilifu. Kila mtu ana sifa na dosari. Ukifahamu ukweli huu utaridhika kabisa na mwenzi wako wa ndoa. Utatambua kwamba jinsi wewe usivyo mkamilifu ndivyo na mwenzi wako wa ndoa asivyo mkamilifu.
Siri ya kuua gugu la kutokuridhika na mwenzi wako wa ndoa ni kutambua kwamba Mungu ndiye aliyekupa mwenzi huyo unayedhani kwamba ana madhaifu. Ukweli ni kwamba Mungu hampi mtu kitu kisichofaa. Mwenzi wako wa ndoa ni chaguo sahihi la Mungu.
(iii) Mpende na kumthamanisha mwenzi wako wa ndoa. Mungu amekuchagulia mwenzi wa ndoa mwenye sifa zote za kuwa mwenzi wako. Ukitokomeza gugu la kutokumpenda au kutokumthamanisha mwenzi wa ndoa uliyepewa na Mungu utampokea kwa shukrani, utamlinda, na kumtunza.
Mwenzi wako wa ndoa ana sifa gani? Ukweli ni kwamba mumeo ni mfalme wako na mkeo ni malkia wako. Na katika jamii iwayo yote watu ambao ni mfalme na malkia hutunzana na kuheshimiana. Pia mfalme na malkia hupokea heshima na matunzo makubwa toka kwa wale wanaowazunguka. Mfalme na malkia wasiotunzana wanakaribisha shida zisizoelezeka.
Thamani ya mwenzi wako wa ndoa, kwa kuwa ametoka kwa Mungu, inazidi thamani ya vito vyote vya thamani katika dunia hii. Mwenzi wako wa ndoa ni almasi. Mwenzi wako wa ndoa ni dhahabu. Mwenzi wako wa ndoa ni lulu. Usiruhusu watu wachezee au kudharau mwenzi wako wa ndoa, ambaye ni ua lako la waridi.
Kumthamanisha mwenzi wako ni kumpenda daima. Ikiwa upendo umepoa au kutoweka kwenye ndoa yako, kaa chini ujiulize swali lifuatalo: ule upendo uliokuwa nao kwa mwenzako wakati wa uchumba bado upo? Ule upendo wa siku za fungate bado upo? Ule upendo uliokuwa ukivuma kwa nguvu kama dhoruba umetokomea wapi? Ikiwa upendo huo haupo, umekwenda wapi? Usiku na mchana tafuta upendo huo na kuurudisha kwenye ndoa yako. Ndoa bila upendo ni sawa na gari lisilokuwa na petroli.
Upendo na kuthamanishana ni sumaku ya kumvuta mwenzi wako wa ndoa. Ni dawa ya kuua gugu liitwalo nyumba ndogo. Tumia dawa hii ili uzuie ndoa yako kubomoka au kusambaratika.
(iv) Kwepa washauri wabaya. Magugu mengi kwenye ndoa huoteshwa na washauri wabaya. Ukikwepa washauri wabaya utakuwa umeng’oa magugu kwenye ndoa yako.
Washauri wabaya ni akina nani? Ni akina Delila na akina Yezebeli ambao huotesha magugu mengi kwenye ndoa, wakisema hili na lile. Ndimi zao hufarakanisha wanandoa badala ya kuwapatanisha. Hubomoa ndoa badala ya kuzijenga.
Usiruhusu washauri wabaya kupanda magugu kwenye ndoa yako. Kataa uchochezi na fitina zao. Usikubali wakuchonganishe na mwenzi wako wa ndoa.
(v) Tawala hisia mbaya. Katika moyo wa mwanadamu kuna hisia nzuri kama vile upendo, huruma, ukarimu, upole, heshima, na unyenyekevu – tukitaja tu chache. Hisia hizi ni tunu za maisha. Kwa hiyo, zidumishe katika ndoa yako.
Hisia mbaya ni zipi? Ni zile ambazo ni magugu ya ndoa. Baadhi ya hisia ambazo ni magugu kwenye ndoa ni wivu, chuki, hasira, ukatili, kiburi, majivuno, na kisasi.
Wanandoa wengine hufikia kiasi cha kuua watu wengine au kujiua wao wenyewe kutokana na gugu linaloitwa wivu wa kimapenzi. Wengine wamechukia na kukasirika pamoja na kubanwa na ukatili kiasi cha kupigana hadharani, kutukanana mbele ya watoto, n.k. Ni vema wanandoa wakakumbuka kwamba hasira ya mwanadamu haitendi haki. Tena walivyosema wahenga, hasira hasara.
Hisia nyingine inayoleta madhara kwenye ndoa ni tamaa mbaya ya mwili. Tamaa hii mbaya humfanya mwanandoa wa kiume kumtamani kila mwanamke anayekutana naye na mwanandoa wa kike kumtamani kila mwanamume anayekutana naye. Gugu hili linaloitwa uzinzi na uasherati limeharibu ndoa nyingi sana, zikiwemo ndoa za watu maarufu kabisa katika jamii.
Dawa ya magugu haya ni nini? Dawa ya magugu yaitwayo wivu, chuki, hasira, ukatili, kiburi, majivuno, na kulipiza kisasi ni kujizuia au kutawala hisia zako.
Kiwatilifu cha kuangamiza gugu la tamaa mbaya ya mwili ni kuitawala tamaa hiyo na kuiridhisha kwenye muktadha unaokubaliwa na Mungu na jamiii, yaani, ndani ya ndoa halali. Ni kukwepa mambo au mazingira yanayochochea tamaa mbaya ya mwili. Ni kutokumwacha mwenzi wako wa ndoa na kujishughulisha na wengine. Ni kuzingatia agizo la kukaa kikamilifu kwenye pingu za maisha, yaani, kifungo cha maisha kiitwacho ndoa.
(vi) Ishi vizuri na wakwe. Wakwe ni akina nani? Mtu anapooa au kuolewa, kuna watu ambao penda asipende huwa na uhusiano wa karibu sana nao. Watu hawa ni kama vile baba na mama mkwe, mashemeji, mawifi, bibi na babu, n.k. Kwa upande mmoja watu hawa ni baraka sana lakini kwa upande mwingine huweza kuwa miiba mikali sana kwenye ndoa, hasa ndoa za wasomi.
Dawa ya kuishi vizuri na watu hawa ni upendo na ukarimu. Nyingine ni busara na uvumilivu. Ni kutawala ulimi na kuchuja maneno. Dawa hizi zikitumika vizuri zitaangamiza kabisa magugu yanayooteshwa na watu hawa.
(vii) Epuka uchafu. Uchafu ni gugu katika ndoa. Kuwa safi ni dawa muhimu sana katika ndoa. Wewe mwanandoa, epuka uchafu wa mwili, uchafu wa mavazi, na uchafu wa nyumba. Epuka uchafu unaosababishwa na harufu mbaya ya sigara na pombe. Oga mara kwa mara ili kuepuka harufu mbaya inayosababishwa na jasho. Ogesha watoto na kuwavisha mavazi nadhifu.
Dawa ya uchafu ni kujipamba au kujipodoa hata baada ya kuoa au kuolewa. Kujipamba wakati wa uchumba peke yake ni kubomoa ndoa yako kwa mikono yako mwenyewe.
Dawa ya kutokomeza uchafu ni kuwa nadhifu kwa njia ya kuvaa nguo zilizofuliwa vizuri na kupigwa pasi. Ni kukwepa kuvaa matambara au mavazi yaliyotatuka. Ni kulala kwenye kitanda chenye mablanketi na shuka safi. Ni kuvaa soksi na nguo za ndani zilizofuliwa. Ni kujipulizia marashi yanayovutia pua ya mwenzi wako wa ndoa. Jipulizie marashi kwenye sehemu zenye uwezekano wa kutoa harufu mbaya, hasa kwenye kwapa na kwenye kinena. Hata hivyo, epuka marashi yasiyokuwa na harufu nzuri.
Dawa ya uchafu ni kudumisha harufu nzuri ya kinywa. Piga mswaki kwa kutumia dawa nzuri ya meno pamoja na kuondoa mabaki ya chakula kwenye meno kila baada ya kula. Dawa ya uchafu ni kunyoa ndevu na kuchana nywele. Ni kukata kucha kwa sababu kufuga kucha ni kufuga uchafu.
(viii) Tawala neema ulizo nazo. Mali na elimu ni neema. Kazi na madaraka ni neema. Afya na sura nzuri ni neema. Nguvu na umbo zuri la mwili ni neema. Neema hizi zote zinapaswa kutumika vizuri katika ndoa. Vinginevyo zitakuwa magugu katika ndoa yako.
Neema zinakuwaje magugu katika ndoa? Neema zikitumika vibaya huwa magugu yanayoleta dhiki katika ndoa. Wanandoa wasiokuwa na busara husikika wakisema: ‘Sikuhitaji tena kwa sababu sina shida ya fedha’ ; ‘Huna manufaa kwangu tena kwa sababu naweza kufanya kila kitu peke yangu’; ‘Baada ya kupata elimu, cheo na mamlaka, wewe kwangu ni takataka tu’; ‘Achana na mimi wee kupe, mrija, na mnyonyaji mkubwa’; ‘Mtu aliyeumbika vizuri kama mimi hawezi kuishi na mtu mwenye sura mbaya kama wewe’. Kauli za jinsi hii ni magugu katika ndoa.
Mwanandoa huhuzunika sana pale anapoambiwa au kurushiwa kauli za kejeli na za kikatili, hasa anapokumbuka jinsi yeye na mwenzi wake anayemkejeli na kumbeza walivyoanza maisha ya ndoa wakiwa hawana kitu. Ni vema mwanandoa ukatambua kwamba maneno ya kujikweza na dharau huwasha kama pilipili. Maneno ya kiburi na masimango huchoma moyo kama mkuki.
(ix) Jiendeleze. Kutokujiendeleza kunakuwaje gugu la ndoa? Hakuna mtu asiyependa mabadiliko chanya. Wala hakuna mtu anayetaka kubakia pale pale wakati wote? Dawa ya gugu hili liitwalo kutokujiendeleza ni kutafuta mbinu mbalimbali za kujiongezea maarifa. Ni kujiongezea elimu. Ni kuboresha utaalamu wako katika mapishi na kazi. Ni kujiendeleza katika taaluma ya mapenzi, kwa kutumia vikolezo vya mapenzi kati ya mume na mke.
(x) Kuwa na kiasi. Mojawapo ya magugu mabaya katika ndoa ni kutokuwa na kiasi katika mambo mbalimbali. Mwanandoa anapaswa kuwa na kiasi katika mambo gani? Anapaswa kuwa na kiasi katika kula, kunywa, kuvaa, na kusema.
Kiasi ni jambo muhimu sana kwa sababu kufanya kitu chochote kwa kupitiliza kuna madhara mengi. Kula kupita kiasi ni kupalilia gugu liitwalo ulafi. Kunywa kupita kiasi ni kualika gugu liitwalo ulevi. Kuvaa kupita kiasi ni kujiingiza kwenye gugu liitwalo anasa. Kusema kupita kiasi ni kuotesha magugu yaitwayo umbeya na masengenyo.
(xi) Omba msamaha. Neno samahani lina umuhimu gani? Neno hili ni dawa nzuri sana ya magugu ya ndoa. Ni dawa ya kutokomeza magugu yanayodhoofisha uhusiano wa wanandoa kama vile kukasirishana, kukoseana, kukwazana, na kochokozana – mambo yanayoumiza au kujeruhi nafsi za wanandoa.
Dawa hii iitwayo samahani, ili iweze kuua magugu ya ndoa, inapaswa itoke moyoni na sio kwenye midomo tu. Kutoa samahani isiyokuwa ya dhati ni sawa na kutibu ugonjwa kwa kutumia nusu dozi. Ni sawa na kunyunyiza dawa ya kuua magugu kwa kurashiarashia tu.
(xii) Shirikiana na Mungu. Kwa nini dawa hii imewekwa mwishoni badala ya mwanzoni mwa mada yetu? Dawa hii imewekwa mwishoni, si kwa lengo la kuonyesha kwamba si muhimu, bali kwa lengo la kuifanya ibebe dawa nyingine zote zilizotangulia kutajwa.
Kumshirikisha Mungu katika kila jambo ni dawa yenye nguvu sana ya kuua magugu yanayosumbua ndoa nyingi. Mwanandoa asiyemfahamu Mungu hawezi kushirikiana na Mungu. Kwa hiyo, kujitahidi kumfahamu Mungu zaidi na zaidi ni dawa yenye nguvu isiyomithalika. Ufahamu pamoja na ushirika wa kweli na Mungu huleta utauwa, hofu ya Mungu, uanana, na uadilifu – zana imara za kupambana na magugu ya ndoa.
Ushirika na Mungu ni dawa ambayo inapaswa kunyunyizwa kwenye magugu ya ndoa kila siku. Kushirikiana na Mungu ni dawa inayonyunyizwa kwa njia ya wanandoa kuomba pamoja, kuabudu pamoja, na kusoma Maandiko Matakatifu pamoja.
Kwa kuwa Mungu ndiye mwasisi wa ndoa, hatakiwi kuachwa pembeni kwenye ndoa iwayo yote. Kwa kuwa mwanamke na mwanamume wameumbwa na Mungu wanapaswa kuishi kwenye ushirika wa karibu kabisa na Mungu kwenye maisha yao ya ndoa. Siri ya kuwa na ndoa itakayodumu maisha yote ya wanandoa ni kwa wanandoa kukaa ndani ya Mungu na Mungu kukaa ndani yao.
Kutokana na ukweli kwamba Mungu ndiye chanzo cha baraka zote katika maisha ya mwanadamu, wanandoa watakaolindwa na kubarikiwa kikamilifu ni wale wanaomtegemea Mungu na kumruhusu kuwa Mwenyekiti wa mipango yao yote.
Kutokushirikiana na Mungu ni gugu la ndoa, na dawa ya gugu hili ni Imani thabiti. Imani thabiti huwafanya wanandoa kujisikia kuwa na usalama, ufanisi, na ulinzi kamili. Wanandoa wanaoshirikiana na Mungu wako chini ya mwamba imara. Mwamba usioshindwa na gugu lolote katika ndoa.
Mpendwa msomaji,
Kuna magugu yoyote kwenye ndoa yako? Ikiwa yapo, nyunyiza dawa iliyotajwa kwenye mada hii, na kusubiri matokeo yake. Mara uonapo matokeo, tafadhali tujulishe kwa kutumia anwani zilizotajwa kwenye blogu yetu.
0 comments:
Post a Comment